Pages

Wednesday, April 24, 2013

HOMA YA UDIWANI JIJI LA ARUSHA YAPANDA (BAVICHA ARUSHA)


JUMANNE, APRILI 23, 2013 05:07 NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MNYUKANO mkali wa kisiasa, unatarajiwa kuibuka tena Juni, mwaka huu, kati ya CCM na CHADEMA, pale vyama hivyo hasimu vitakapokutana kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani Jimbo la Arusha Mjini. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza Juni 21, mwaka huu, kufanyika chaguzi za marudio kote nchini, ambapo Arusha kata nne zinatarajiwa kutimua vumbi.

Kufanyika kwa uchaguzi huo, kumekuja baada ya CHADEMA kuwatimua madiwani wake, baada ya kwenda kinyume na maelekezo ya Chama.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha, Efatha Nanyaro, pamoja na kuzungumzia maandalizi ya uchaguzi huo, aliituhumu NEC na Serikali kutoijumuisha Kata ya Sombetini.

Nanyaro ambaye ni Diwani wa Kata ya Levolosi, alisema kipindi ambacho NEC ilikuwa inasita kutangaza uchaguzi huo wao walikuwa wakiendelea na maandalizi.

“Tuna uhakika mkubwa wa kushinda kata zote na hili halina ubishi, mpaka sasa wagombea zaidi ya 55, wamejitokeza kuomba kwa kata zote.

“Hatuna uhaba wa rasilimali watu, tumekuwa tukitoa mafunzo ya uongozi kwa muda mrefu, hawa watu ni wasomi wenye nia ya kuitumikia nchi yao,” alisema Nanyaro.

Alizitaja kata zitakazoshiriki uchaguzi na idadi ya wagombea waliojitokeza kuwa ni Kata ya Kimandolu (15), Elerai (18), Kaloleni (10) na Kata ya Themi (12).

Alipoulizwa wingi wa wagombea hao, kama unaweza kuleta mvutano kwenye uteuzi wa jina moja, Nanyaro alisema suala hilo ni vigumu kutokea kwa sasa.

“Mfumo wetu wa kupata viongozi upo wazi kabisa, ni vugumu kuibua makundi, hatutarajii mgogoro na mapema tunatarajia kuanza mchakato wa mgombea kwa kila kata,” alisema Nanyaro.

Akizungumzia Kata ya Sombetini, ambayo diwani wake, Alfonsi Mawazo aliyekuwa CCM alihamia CHADEMA, alisema Serikali imesita kuijumuisha kata hiyo kutokana na kutambua kuwa ni ngome ya CHADEMA.

“Ile ni ngome ya CHADEMA, hata tusipofanya kampeni tutashinda na CCM, Serikali na NEC, wameogopa kwa sababu wanajua tukiichukua na Sombetini basi Halmashauri itaongozwa na CHADEMA.

“Kauli ya Mawazo hakuandika barua ya kujiuzulu haina mashiko, hata kama hakuandika barua, ana zaidi ya vikao vitatu hajahudhuria, hicho tu ni kigezo tosha cha kumfukuzisha udiwani,” alisema Nanyaro.

Katika uchaguzi wa hivi karibuni, CHADEMA kilifanikiwa kunyakua kata nyingine iliyokuwa ikiongozwa na CCM ya Daraja Mbili, baada ya diwani wake kufariki dunia mwaka jana.

0 comments:

Post a Comment