Jumatano, Februari 06, 2013 04:42 Na Esther Mbussi
MWENENDO wa mambo ndani ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (BAVICHA) unaendelea kuwa tete, kutokana na vita ya makundi
yanayotofautiana kimsimamo na kimtizamo kuendelea kushika kasi,
Mwenyekiti wa Baraza hilo, John
Heche, alipotangaza kuwatimua kundini baadhi ya wanachama,akiwemo Makamu Mwenyekiti wake, Juliana Shonza.
Uamuzi huo uliotangazwa na Heche unapingwa na Shonza,ambaye amekuwa
akieleza kuwa yeye bado ni Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA na kwamba
anaendelea na shughuli zake za kiuongozi ndani ya jumuiya hiyo kama
kawaida, kwa sababu taratibu za kumtimua zilikuwa batili.
Ili
kupata msimamo wa Shonza kuhusu hatma yake ya kisiasa baada ya tangazo
la kutimuliwa kwake, Mtanzania Jumatano limefanya naye mahojiano ya ana
kwa ana ambapo alisisitiza kauli yake hiyo na kutumia fursa hiyo ya
mahojiano kutangaza kuwa atawania uenyekiti wa BAVICHA katika uchaguzi
ujao wa viongozi wa Jumuiya za Chadema.
Sambamba na hilo, Shonza pia alitangaza kuwa ni mfuasi wa Zitto kisiasa na kwamba atamuunga mkono iwapo atatekeleza uamuzi
wake wa kuomba kuteuliwa na Chadema kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mtanzania Jumatano: Umevuliwa uongozi wa BAVICHA. Ukiwa nje ya BAVICHA,
unautizamaje mwenendo wako wa kisiasa ukilinganisha na ulipokuwa
kiongozi?
Shonza: Mimi siko nje ya Bavicha,mnakosea sana
kuamini hivyo.Naomba nieleweke vizuri kwamba mimi bado ni Makamu
Mwenyekiti wa Bavicha kwa sababu niliwekwa kwa misingi ya Katiba na
misingi ya Katiba pekee ndiyo inayoweza kuniondoa.
Kiongozi aliyechaguliwa kikatiba hawezi kuondolewa kwa matakwa ya mtu kama Wegesa Suguta,anayetumika kama daraja la
mabosi wake kutekeleza matakwa yao na ndiyo maana hata kushinda kwake alishinda kimagumashi. Aliwekwa hapo kwa nguvu ili
awatumikie waliomuweka badala ya Jumuiya ya vijana na chama kwa ujumla.
Mtanzania Jumatano: Jina hili la Wegesa Suguta ni geni katika safu za
uongozi wa Chadema kwa ujumla, hapa unamaanisha ni nani huyu na ana
nafasi gani ndani ya Bavicha au Chadema?
Shonza: Ni huyo ambaye nyie mnamwita John Heche.
Mtanzania Jumatano: Hili ni jina lake halisi au umembatiza wewe?
Shonza: Mimi nadhani swali hilo aulizwe yeye mwenyewe.Muulizeni hilo la
John Heche kalipata wapi? Mimi namjua kwa jina la Wegesa Suguta ambalo
liko kwenye vyeti vyake. Nawaachia kazi hiyo.
Mtanzania
Jumatano: Unasema wewe bado ni Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, unamaanisha
Heche alikosea kutoa tamko la kukuondoa madarakani na kukufukuza
uanachama?
Shonza: Ndiyo, na hili liko wazi kabisa. Siyo siri kwamba Wegesa (Heche) anaonekana ana sauti sana ndani ya Baraza kwa sababu
kuna vinara ndani ya chama ambao wako nyuma yake na hawa ndiyo waliomuweka hapo alipo ili awatumikie na kutimiza matakwa
yao. Na ndiyo maana unapozungumzia udhaifu wa Wegesa (Heche) hutaacha
kumuelezea kwamba ni kiongozi aliyeshindwa kuwaunganisha vijana ndani ya
baraza na vijana ndani ya chama wanafahamu hili.
Wegesa
(Heche) ana uwezo mdogo wa kiuongozi unaomfanya achukue maamuzi
yasiyofuata Katiba ya chama na mwongozo wa baraza. Katika mazingira kama
hayo,tegemea kuungwa mkono na watu wasiojitambua lakini kwa watu
wanaojitambua ni ngumu kumuunga mkono Wegesa (Heche).
Hata
historia inamhukumu kwani katika uchaguzi wa mwaka 2009 wa Bavicha
aligombea akagalagazwa vibaya na David Kafulila, lakini kutokana na
ukweli kwamba Kafulila hakuwa chagua la viongozi wakuu ndani ya chama
kwa sababu misimamo yake thabiti na uwezo alionao, uchaguzi ule
ukavurugwa na Kafulila akaambulia kufukuzwa.
Uchaguzi huo baada
ya kuingia ‘kidudumtu’ uliitishwa tena mwaka 2011 na Wegesa (Heche)
aliyekuwa akipiganiwa na vigogo wa chama alishinda kwa mbinde sana baada
ya vijana watatu ambao ni Mtela Mwampamba, Habib Mchange na Nyakarungu
wenye uwezo kuondolewa, achana na Ben Saanane aliyeenguliwa kimkakati,
lakini bado Wegesa (Heche) alishinda kwa asilimia 51 tu.
Mtanzania Jumatano: Kwa hiyo wewe ni kiongozi unayeongoza kundi lipi? Maana Bavicha imeshatangaza haikutambui.
Shonza: Mimi ni kiongozi, kama yupo anayesema hanitambui basi huyo ni Wegesa (Heche) na wenzake wanaoogopa changamoto
mpya ndani ya chama na kiongozi ni yule anayetambulika kikatiba, sawa! Mimi natambulika kikatiba, alisema nimeondolewa alikiuka
misingi ya Katiba, kwa hiyo sitishwi na maneno ya vibaraka wa aina ya Wegesa (Heche) kwamba eti mimi Shonza si mwanachama
au kiongozi. Thats nonsense. Na ndiyo maana viongozi wenye kujua
misingi ya kikatiba huko mikoani wananitambua kama kiongozi wao, bado
nashirikiana nao na sitaacha kushirikiana nao.
Tunajenga chama,
hatutaki majungu sisi wala kufukuzana, kisa hofu inayotokana na uwezo
mdogo wa kiuongozi unaomfanya mhusika kuhofia kupokwa cheo alichonacho.
Mtanzania Jumatano: Zipo tuhuma kwamba ulishiriki kuanzisha Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) na pia ni mshirika wa
makundi ya Masalia na PM7-pindua Mbowe, tuhuma hizi unazizungumziaje?
Shonza: Nilishasema tangu awali na hata kwenye tamko langu nililisema hili kwamba mpaka sasa sizifahamu tuhuma zangu. Siwezi
jibu tuhuma zilizotolewa na kiongozi ‘kilaza’ kwenye magazeti, kwani nami nitadhihirisha kuwa ni kilaza kama yeye au wao maana
chama kina utaratibu wake wa kuwasilishiana tuhuma kwa viongozi na
wanachama wake. Na ndiyo maana hata wao wameogopa kuniandikia hizo
tuhuma maana wanajua fika kuwa ni za uongo, uzushi na uzandiki mtupu.
Hata huo ushahidi wanaosema wanao ni uongo na kujijaza upepo tu sawa na
kupiga ngoma na kucheza mwenyewe. Wamezoea kuwadanganya Watanzania
kwamba wana ushahidi, wana ushahidi wakati hawana chochote, wanacheza na
akili za watu ili tu waaminiwe upesi. Mimi ninawaomba waache tabia ya
kuwadanganya wananchi kwamba wana ushahidi, sijui intelijensia kumbe
wanapeleka majungu na umbea tu. Ni aibu kuwa na kiongozi mpika majungu,
msikiliza majungu na anayeendesha chama kimajungu.
Sasa kwa
ufupi tu ni kwamba mimi bado ni mwana Chadema na kupitia mahojiano haya,
natangaza rasmi ili Watanzania wote wasikie, kwamba nitagombea
Uenyekiti waBAVICHA mwaka huu. Mimi ni kamanda na kamanda hakimbii vita
hata siku moja.
Mtanzania Jumatano: Unatangaza uamuzi mzito
sana huo ukiwa katika mgogoro na viongozi wako, itakuwaje ukikataliwa
kugombea.Utachukua hatua gani, utahama chama kama ambavyo imetokea kwa
wanasiasa wengine wengi waliokutangulia au utachukua hatua gani?
Shonza: Wakifanya hivyo watakuwa wameamua ‘kubaka’ demokrasia ndani ya
chama na chama kisicho na demokrasia ni hatari kwa mustakabali wa nchi
yetu. Watanzania na wana Chadema wataona na wataamua iwapo itakuwa
hivyo. Lakini hata ikiwa hivyo, sitakaa nikahama chama, nitapambana
nikiwa ndani ya chama, nitapigania demokrasia.
Mimi ninaamini
hakuna haja ya kukimbia changamoto na ndiyo maana hata wenzangu
ninaodaiwa kuvuliwa nao uanachama kwa mujibu wa tangazo la Wegesa
(Heche) walipochujwa kutogombea Uenyekiti Bavicha katikati ya uchaguzi,
hawakuondoka Chadema.
Mtanzania Jumatano: Vipi kuhusu tuhuma kwamba unatumiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,Zitto Kabwe kukihujumu chama?
Shonza: Mimi siyo mtu wa kutumiwa, bali ninajituma mwenyewe kwa sababu
ninajitambua, sishikiwi akili na mtu. Situmiwi na Zitto wala yeyote
ndani ya chama, isipokuwanimekuwa nikishirikiana naye kwa karibu katika
shughuli za ujenzi wa chama kwa sababu nyingi,kwanza ni kiongozi kijana
ambaye ana uwezo mkubwa wa kiuongozi na amekuwa chimbuko la vijana wengi
kujiunga na upinzani, nikiwemo mimi mwenyewe.
Pili ni kiongozi
aliyekaribu sana na viongozi wote wa Baraza la Vijana bila kubagua kama
baadhi ya viongozi wa chama wanavyofanya.
Kwa mfano ni
kiongozi pekee aliyetoa gari lake bure litumike kwa shughuli za ujenzi
wa baraza japo Wegesa (Heche) amelifanya gari hilo la kwake, ufisadi
mwingine huu kutumia mali ya baraza kwa matumizi yake binafsi.
Pia, siku zote nimekuwa nikivutiwa na siasa za Zitto zilizojaa weledi
mkubwa katika namna ya kujenga na kusimamia hoja, kuwa na msimamo na
kutoyumbishwa.
Zitto si kiongozi wa hovyo kama ambavyo gazeti la kipropaganda la Chadema limekuwa likimchafua, kwamba anamiliki mtandao wa
vijana wanaotaka kuharibu chama. Tatizo ni kwamba ukiwa na uwezo na msimamo wa kusimamia kile unachokiamini, ‘future’ yako
Chadema inakuwa mashakani. Ndicho kilichomkuta marehemu Chacha Wangwe, Kafulila, Walid Kaborou na wengine wengi.
Pamoja na haya bado si mwisho, wako wengine watakuja kuyaongea haya
tunayoyaongea sisi sasa, maana hata sisi wanaotuita masalia atukuwa wa
kwanza kufukuzwa bila kufuata misingi ya kikatiba.
Kwa hiyo
mimi ni muumini wa siasa za Zitto, lakini hanitumii na niweke wazi
kabisa kwamba endapo akigombea Urais 2015, kama ilivyo azma
yake,nitamuunga mkono kwa asilimia100.
Mtanzania Jumatano: Unazionaje siasa za ndani ndani ya Chadema kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Shonza: Bado kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya 2015 ili tuweze
kuchukua nchi, hasa maeneo ya vijijini, bila kuwasahau na kuwaacha
wanawake nyuma, maana ndiyo wadau wakubwa na ndiyo wapiga kura wakubwa.
Lakini jambo la muhimu ni chama ‘kirecruit’ wanawake wengi na kiwatie
moyo badala ya kuwakatisha tamaa.
Lakini jambo la muhimu zaidi
ambalo ni lazima viongozi wakuu wa chama wakubali kubadilika
tunapoelekea mwaka 2015 ni hili linalohusu uadilifu wao.
Tunawatuhumu viongozi wengine kwa ufisadi, tunawatangazia Watanzania
kuwa uadilifu wa viongozi wa vyama vingine ni wa kutiliwa shaka wakati
viongozi ndani ya Chadema uadilifu wao una madoa mengi meusi. Hili
litatugharimu kama chama.
Viongozi wakubali kujisahihisha,
Chadema ni chama cha siasa cha Watanzania wote, huo ndiyo msingi wa
kuanzishwa kwake, na siyo chama cha kuwanufaisha wachache wanaojua
kuteka akili za wengine kwa sababu wamewachoka waliopo madarakani.
Siasa za ndani ya Chadema ni siasa zilizogubikwa na uviziaji wa
demokrasia, ubaguzi wa ukanda na ukabila. Hili ni tatizo ambalo siku
Watanzania na wanachama wa Chadema wakiligundua, chama hiki kitaporomoka
na kuwa kama vingine vilivyopata kuwa maarufu halafu vikaporomoka kwa
kasi ya ajabu.
Mfumo wa sasa wa uendeshwaji wa chama wa mfano
wa Saccos haufai. Ni lazima uachwe. Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa,
kajikopesha Sh. milioni 140 ambayo ni michango ya wanachama na wakati
huo huo analipwa donge nono la mshahara wa zaidi ya Sh. milioni saba kwa
mwezi pamoja na marupurupu mengine. Hili haliwezekani kunyamaziwa kwa
sababu fedha hizi ni za wanachama.
Ni aibu kwa kiongozi kama
Dk. Slaa kuudanganya umma wa Watanzania kuwa amekopa Sh. milioni 20
wakati nafsi yake anajua kuwa si kweli. Wako wapi wakaguzi wa hesabu za
fedha ndani ya vyama hivi vya siasa!
Inafika mahala tunashindwa
kujua kama ni kweli Dk. Slaa wa sasa ndiye yule aliyesoma orodha ya
mafisadi pale Mwembe Yanga au la! Kwa sababu matendo yake hayaendani na
mahubiri yake.
Bado tuna kazi kubwa ndani ya chama, lakini ninaamini tutajisafisha tu. Acha niwajibike bwana, siku nyingine nihoji.
chanzo:Mtanzania/Juliana shonza